KAMISHENI ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO) imeiweka hadharani mikanda itakayogombaniwa katika mapambano ya Tubing wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati yatakayofanyika Julai 22, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem, Dar.
Katika mapambano hayo ya kimataifa yatakayorushwa mubashara na Kituo cha Global TV Online kupitia webiste yake ya www.globaltvtz. com, Bondia wa Tanzania, Francis Miyeyusho ‘Chichi Mawe’ atapambana na Israel Kamwamba wa Malawi.
Pambano lingine litakuwa ni kati ya Idd Pialali dhidi ya Regin Champion raia wa DR Congo, wakati Nasibu Ramadhan ‘Pacman’ atacheza na Tinashe Mwadziwana kutoka Zimbabwe. Mapambano hayo yote ni ya raundi kumi.
Rais wa TPBO, Yassin Abdallah ‘Ustaadh’, ameitambulisha mikanda itakayogombaniwa katika mapambano hayo huku akithibitisha uwepo wa Balozi wa Malawi wa hapa nchini, Hawa Ndilowe kwenye pambano hilo.
“Maandalizi ya mapambano ya kimataifa, kati ya mabondia wa kutoka DR Congo, Malawi na Zimbabwe ambao watapigana na mabondia wetu hapa, yamekamilika. Kila kitu kimeshakuwa sawa na wameshapata barua maalum kutoka katika mashirikisho ya nchi zao.
“Huo ndiyo mfumo wa ngumi za kulipwa unavyokuwa, bondia anatakiwa apate ridhaa na kibali cha kwenda kupigana nje ya nchi kutoka kwa kamisheni, chama au shirikisho la ngumi za kulipwa ndani ya nchi yake.